Zaburi  
KITABU CHA KWANZA 
 1
(Zaburi 1–41) 
Furaha Ya Kweli 
 1 Heri mtu yule ambaye 
haendi katika shauri la watu waovu, 
wala hasimami katika njia ya wenye dhambi, 
au kuketi katika baraza la wenye mizaha. 
 2 Bali huifurahia sheria ya Bwana, 
naye huitafakari hiyo sheria usiku na mchana. 
 3 Mtu huyo ni kama mti uliopandwa 
kando ya vijito vya maji, 
ambao huzaa matunda kwa majira yake 
na majani yake hayanyauki. 
Lolote afanyalo hufanikiwa. 
Huzuni Ya Waovu 
 4 Sivyo walivyo waovu! 
Wao ni kama makapi 
yapeperushwayo na upepo. 
 5 Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu, 
wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki. 
 6 Kwa maana Bwana huziangalia njia za mwenye haki, 
bali njia ya waovu itaangamia.