46
Miungu Ya Babeli 
 1 Beli anasujudu hadi nchi, Nebo anainama; 
sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo. 
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea, 
mzigo kwa waliochoka. 
 2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini; 
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu, 
wote wanakwenda utumwani pamoja. 
 3 “Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo, 
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli, 
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba, 
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu. 
 4 Hata mpaka wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye, 
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi. 
Nimewahuluku, nami nitawabeba, 
nitawasaidia ninyi na kuwaokoa. 
 5 “Mtanilinganisha na nani, au mtanihesabu kuwa sawa na nani? 
Ni nani mtakayenifananisha naye ili tuweze kulinganishwa? 
 6 Wengine humwaga dhahabu kutoka kwenye mifuko yao, 
na kupima fedha kwenye mizani; 
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu, 
kisha huisujudia na kuiabudu. 
 7 Huiinua mabegani na kuichukua; 
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo. 
Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale. 
Ingawa mtu huililia, haimjibu; 
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake. 
 8 “Kumbukeni hili, litieni akilini, 
liwekeni moyoni, enyi waasi. 
 9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale; 
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine; 
mimi ndimi Mungu, 
wala hakuna mwingine aliye kama mimi. 
 10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo, 
naam, tangu zamani za kale, 
mambo ambayo hayajatendeka. 
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama, 
nami nitatenda mapenzi yangu yote. 
 11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye; 
kutoka nchi ya mbali, 
mtu atakayetimiza kusudi langu. 
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza; 
lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda. 
 12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu, 
ninyi mlio mbali na haki. 
 13 Ninaleta haki yangu karibu, 
haiko mbali; 
wala wokovu wangu hautachelewa. 
Nitawapa Sayuni wokovu, 
Israeli utukufu wangu.