3
Mashahidi Waitwa Dhidi Ya Israeli 
 1 Sikilizeni neno hili alilosema Bwana dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri: 
 2 “Ni ninyi tu niliowachagua 
kati ya jamaa zote za dunia; 
kwa hiyo nitawaadhibu 
kwa ajili ya dhambi zenu zote.” 
 3 Je, watu wawili hutembea pamoja 
wasipokubaliana kufanya hivyo? 
 4 Je, simba hunguruma katika kichaka 
wakati hana mawindo? 
Aweza kuvuma katika pango 
wakati ambao hajakamata chochote? 
 5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini 
ambapo hajategewa chambo? 
Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini 
wakati ambapo hakuna chochote cha kunasa? 
 6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari, 
watu hawatetemeki? 
Mji upatwapo na maafa, 
je, si Bwana amesababisha? 
 7 Hakika Bwana Mwenyezi hatafanya neno lolote 
bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. 
 8 Simba amenguruma: 
je, ni nani ambaye hataogopa? 
Bwana Mwenyezi ametamka: 
je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii? 
 9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi 
na katika ngome za Misri: 
“Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria; 
angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake, 
na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.” 
 10  Bwana asema: “Hawajui kutenda lililo jema, 
wale ambao hujilundikia nyara 
na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.” 
 11 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi: 
“Adui ataizingira nchi; 
ataangusha chini ngome zenu 
na kuteka nyara maboma yenu.” 
 12 Hili ndilo asemalo Bwana: 
“Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba 
vipande viwili tu vya mfupa wa mguu 
au kipande cha sikio, 
hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa, 
wale wakaao Samaria 
kwenye kingo za vitanda vyao, 
na katika Dameski 
kwenye viti vyao vya fahari.” 
 13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote. 
 14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake, 
nitaharibu madhabahu za Betheli; 
pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali 
na kuanguka chini. 
 15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika, 
pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi; 
nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu 
na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,” 
asema Bwana.