47
Ujumbe Kuhusu Wafilisti 
 1 Hili ndilo neno la Bwana lililomjia nabii Yeremia kuhusu Wafilisti, kabla Farao hajaishambulia Gaza: 
 2 Hili ndilo asemalo Bwana: 
“Tazama jinsi maji yanavyoinuka huko kaskazini, 
yatakuwa mafuriko yenye nguvu sana. 
Yataifurikia nchi na vitu vyote vilivyomo ndani yake, 
miji na wale waishio ndani yake. 
Watu watapiga kelele; 
wote waishio katika nchi wataomboleza 
 3 kwa sauti ya kwato za farasi waendao mbio, 
kwa sauti ya magari ya adui 
na mngurumo wa magurudumu yake. 
Baba hawatageuka kuwasaidia watoto wao, 
mikono yao italegea. 
 4 Kwa maana siku imewadia 
kuwaangamiza Wafilisti wote 
na kuwakatilia mbali walionusurika wote 
ambao wangeweza kusaidia Tiro na Sidoni. 
Bwana anakaribia kuwaangamiza Wafilisti, 
mabaki toka pwani za Kaftori.* Kaftori ndio Krete. 
 5 Gaza atanyoa kichwa chake katika kuomboleza, 
Ashkeloni atanyamazishwa. 
Enyi mabaki kwenye tambarare, 
mtajikatakata wenyewe mpaka lini? 
 6 “Mnalia, ‘Aa, upanga wa Bwana, 
utaendelea mpaka lini ndipo upumzike? 
Rudi ndani ya ala yako; 
acha na utulie.’ 
 7 Lakini upanga utatuliaje 
wakati Bwana ameuamuru, 
wakati ameuagiza kuishambulia Ashkeloni 
pamoja na pwani yake?”