3
 1 Usiku kucha kwenye kitanda changu 
nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye; 
nilimtafuta, lakini sikumpata. 
 2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini, 
katika barabara zake na viwanja; 
nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye. 
Kwa hiyo nilimtafuta lakini sikumpata. 
 3 Walinzi walinikuta 
walipokuwa wakizunguka mji. 
Nikawauliza, “Je, mmemwona 
yule moyo wangu umpendaye?” 
 4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita 
nilimpata yule moyo wangu umpendaye. 
Nilimshika na sikumwachia aende 
mpaka nilipomleta katika nyumba ya mama yangu, 
katika chumba cha yule aliyenichukua mimba. 
 5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza 
kwa paa na kwa ayala wa shambani: 
Msichochee wala kuamsha mapenzi 
hata yatakapotaka yenyewe. 
Shairi La Tatu 
Mpenzi 
 6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani 
kama nguzo ya moshi, 
anayenukia manemane na uvumba 
iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote 
vya mfanyabiashara? 
 7 Tazama! Ni gari la Solomoni 
lisindikizwalo na mashujaa sitini, 
walio wakuu sana wa Israeli, 
 8 wote wamevaa panga, 
wote wazoefu katika vita, 
kila mmoja na upanga wake pajani, 
wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku. 
 9 Mfalme Solomoni alijitengenezea gari; 
alilitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni. 
 10 Nguzo zake alizitengeneza kwa fedha, 
kitako chake kwa dhahabu. 
Kiti chake kilipambwa kwa zambarau, 
gari lake likanakshiwa njumu kwa upendo 
na binti za Yerusalemu. 
 11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni, 
mkamtazame Mfalme Solomoni akiwa amevaa taji, 
taji ambalo mama yake alimvika 
siku ya arusi yake, 
siku ambayo moyo wake ulishangilia.