9
Adhabu Kwa Israeli 
 1 Usifurahie, ee Israeli; 
usishangilie kama mataifa mengine. 
Kwa kuwa hukuwa 
mwaminifu kwa Mungu wako; 
umependa ujira wa kahaba kwenye kila sakafu 
ya kupuria nafaka. 
 2 Sakafu za kupuria nafaka na mashinikizo ya kukamulia divai 
havitalisha watu, 
divai mpya itawapungukia. 
 3 Hawataishi katika nchi ya Bwana, 
Efraimu atarudi Misri 
na atakula chakula 
kilicho najisi huko Ashuru. 
 4 Hawatammiminia Bwana sadaka ya divai 
wala dhabihu zao hazitampendeza. 
Dhabihu kama hizo zitakuwa kwao 
kama mkate wa waombolezaji; 
nao wote wazilao watakuwa najisi. 
Chakula hiki kitakuwa kwa ajili yao wenyewe; 
kisije katika Hekalu la Bwana. 
 5 Mtafanya nini katika siku ya sikukuu zenu zilizoamriwa, 
katika siku za sikukuu za Bwana? 
 6 Hata ikiwa wataokoka maangamizi, 
Misri atawakusanya, 
nayo Memfisi* Memfisi kwa Kiebrania ni Nofu. itawazika. 
Hazina zao za fedha zitasongwa na michongoma, 
nayo miiba itafunika mahema yao. 
 7 Siku za adhabu zinakuja, 
siku za malipo zimewadia. 
Israeli na afahamu hili. 
Kwa sababu dhambi zenu ni nyingi sana 
na uadui wenu ni mkubwa sana, 
nabii anadhaniwa ni mpumbavu, 
mtu aliyeongozwa na Mungu 
anaonekana mwendawazimu. 
 8 Nabii, pamoja na Mungu wangu, 
ndiye mlinzi juu ya Efraimu, 
hata hivyo mitego inamngojea 
katika mapito yake yote, 
na uadui katika nyumba ya Mungu wake. 
 9 Wamezama sana katika rushwa, 
kama katika siku za Gibea. 
Mungu atakumbuka uovu wao 
na kuwaadhibu kwa ajili ya dhambi zao. 
 10 “Nilipompata Israeli, ilikuwa kama 
kupata zabibu jangwani; 
nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona 
matunda ya kwanza katika mtini. 
Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu 
kwa ile sanamu ya aibu, 
nao wakawa najisi 
kama kitu kile walichokipenda. 
 11 Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: 
hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba, 
hakuna kutunga mimba. 
 12 Hata wakilea watoto, 
nitamuua kila mmoja. 
Ole wao 
nitakapowapiga kisogo! 
 13 Nimemwona Efraimu, kama Tiro, 
aliyeoteshwa mahali pazuri. 
Lakini Efraimu wataleta 
watoto wao kwa mchinjaji.” 
 14 Wape, Ee Bwana, 
je, utawapa nini? 
Wape matumbo ya kuharibu mimba 
na matiti yaliyokauka. 
 15 “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, 
niliwachukia huko. 
Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, 
nitawafukuza katika nyumba yangu. 
Sitawapenda tena, 
viongozi wao wote ni waasi. 
 16 Efraimu ameharibiwa, 
mzizi wao umenyauka, 
hawazai tunda. 
Hata kama watazaa watoto, 
nitawachinja watoto wao 
waliotunzwa vizuri.” 
 17 Mungu wangu atawakataa 
kwa sababu hawakumtii; 
watakuwa watu wa kutangatanga 
miongoni mwa mataifa.