5
Hukumu Dhidi Ya Israeli 
 1 “Sikieni hili, enyi makuhani! 
Kuweni wasikivu, enyi Waisraeli! 
Sikieni, ee nyumba ya mfalme! 
Hukumu hii ni dhidi yenu: 
Mmekuwa mtego huko Mispa, 
wavu uliotandwa juu ya Tabori. 
 2 Waasi wamezidisha sana mauaji. 
Mimi nitawatiisha wote. 
 3 Ninajua yote kuhusu Efraimu, 
Israeli hukufichika kwangu. 
Efraimu, sasa umegeukia ukahaba, 
Israeli amenajisika. 
 4 “Matendo yao hayawaachii 
kurudi kwa Mungu wao. 
Roho ya ukahaba imo ndani ya mioyo yao, 
hawamkubali Bwana. 
 5 Kiburi cha Israeli kinashuhudia dhidi yao; 
Waisraeli, hata Efraimu, 
wanajikwaa katika dhambi zao; 
pia Yuda atajikwaa pamoja nao. 
 6 Wakati wanapokwenda na makundi yao 
ya kondoo na ngʼombe 
kumtafuta Bwana, 
hawatampata; 
yeye amejiondoa kutoka kwao. 
 7 Wao si waaminifu kwa Bwana; 
wamezaa watoto haramu. 
Sasa sikukuu zao za Mwandamo wa Mwezi 
zitawaangamiza wao 
pamoja na mashamba yao. 
 8 “Pigeni tarumbeta huko Gibea, 
baragumu huko Rama. 
Paza kilio cha vita huko Beth-Aveni,* Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka. 
ongoza, ee Benyamini. 
 9 Efraimu ataachwa ukiwa 
katika siku ya kuadhibiwa. 
Miongoni mwa makabila ya Israeli 
ninatangaza lile ambalo halina budi kutukia. 
 10 Viongozi wa Yuda ni kama wale 
wanaosogeza mawe ya mpaka. 
Nitamwaga ghadhabu yangu juu yao 
kama mafuriko ya maji. 
 11 Efraimu ameonewa, 
amekanyagwa katika hukumu 
kwa kuwa amekusudia kufuatia sanamu. 
 12 Mimi ni kama nondo kwa Efraimu, 
na kama uozo kwa watu wa Yuda. 
 13 “Wakati Efraimu alipoona ugonjwa wake, 
naye Yuda vidonda vyake, 
ndipo Efraimu alipogeukia Ashuru, 
na kuomba msaada kwa mfalme mkuu. 
Lakini hawezi kukuponya, 
wala hawezi kukuponya vidonda vyako. 
 14 Kwa maana nitakuwa kama simba kwa Efraimu, 
kama simba mkubwa kwa Yuda. 
Nitawararua vipande vipande na kuondoka; 
nitawachukua mbali, 
na hakuna wa kuwaokoa. 
 15 Kisha nitarudi mahali pangu 
mpaka watakapokubali kosa lao. 
Nao watautafuta uso wangu; 
katika taabu yao watanitafuta kwa bidii.”