10
 1 Kama vile nzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato, 
ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima. 
 2 Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume, 
lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto. 
 3 Hata anapotembea barabarani, 
mpumbavu hukosa ufahamu 
na kudhihirisha kwa kila mmoja 
jinsi alivyo mpumbavu. 
 4 Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako, 
usiache mahali pako, 
utulivu huweza kuzuia makosa mengi. 
 5 Kuna ubaya niliouona chini ya jua, 
aina ya kosa litokalo kwa mtawala: 
 6 Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za juu, 
wakati matajiri hushika nafasi za chini. 
 7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, 
wakati wakuu wakitembea 
kwa miguu kama watumwa. 
 8 Yeye achimbaye shimo 
aweza kutumbukia ndani yake, 
yeyote abomoaye ukuta 
anaweza kuumwa na nyoka. 
 9 Yeyote apasuaye mawe 
inawezekana yakamuumiza, 
yeyote apasuaye magogo 
inawezekana yakamuumiza. 
 10 Kama shoka ni butu 
na halikunolewa, 
nguvu nyingi zinahitajika, 
lakini ustadi utaleta mafanikio. 
 11 Kama nyoka akiuma kabla ya kufanyiwa uaguzi, 
mwaguzi hatahitajika tena. 
 12 Maneno yatokayo kinywani mwa mtu mwenye hekima 
yana neema, 
bali mpumbavu huangamizwa 
na midomo yake mwenyewe. 
 13 Mwanzoni maneno yake ni upumbavu, 
mwishoni ni wazimu mbaya, 
 14 naye mpumbavu huzidisha maneno. 
Hakuna yeyote ajuaye linalokuja, 
ni nani awezaye kueleza ni jambo gani 
litakalotokea baada yake? 
 15 Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe, 
hajui njia iendayo mjini. 
 16 Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa 
na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi. 
 17 Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako ni wa uzao wenye kuheshimika 
na ambayo wakuu wako hula chakula kwa wakati unaofaa: 
ili kupata nguvu na si kwa ajili ya ulevi. 
 18 Kama mtu ni mvivu paa la nyumba huinama, 
kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja. 
 19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, 
nao mvinyo hufurahisha maisha, 
lakini fedha ni jawabu la mambo yote. 
 20 Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako, 
au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala, 
kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako, 
naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.