Zaburi 4
Sala Ya Jioni Ya Kuomba Msaada 
Kwa mwimbishaji. Kwa ala za nyuzi za muziki. Zaburi ya Daudi. 
 1 Nijibu nikuitapo, 
Ee Mungu wangu mwenye haki! 
Nipumzishe katika shida zangu; 
nirehemu, usikie ombi langu. 
 2 Enyi watu, mtabadilisha utukufu wangu 
kuwa aibu mpaka lini? 
Mtapenda udanganyifu 
na kufuata miungu ya uongo mpaka lini? 
 3 Fahamuni hakika kwamba Bwana amewatenga 
wale wamchao kwa ajili yake; 
Bwana atanisikia nimwitapo. 
 4 Katika hasira yako, usitende dhambi. 
Mkiwa vitandani mwenu, mtulie kimya 
mkiichunguza mioyo yenu. 
 5 Toeni dhabihu zilizo haki; 
mtegemeeni Bwana. 
 6 Wengi wanauliza, “Ni nani awezaye 
kutuonyesha jema lolote?” 
Ee Bwana, tuangazie nuru ya uso wako. 
 7 Wewe umejaza moyo wangu kwa furaha kubwa 
kuliko watu waliopata nafaka na divai kwa wingi. 
 8 Nitajilaza chini na kulala kwa amani, 
kwa kuwa wewe peke yako, Ee Bwana, 
waniwezesha kukaa kwa salama.